Monday, April 04, 2016

TFF KWA HILI MMECHEMSHA TENA SANAAAA..NA KAMATI ZENU HIZO...


‘Jambo moja katika mambo yasiyo na maana ni kutangaza habari ya kosa la mtu mdogo kwa sababu tendo lake ni kama tendo la mwendawazimu ambalo wenye akili timamu hawawezi kulipatiliza’ Wakati mwingine maamuzi yanayotolewa katika kamati mbalimbali za TFF (Shirikisho la mpira wa miguu nchini) yanachekesha sana, lakini kwa namna ya kusaka maendeleo ya mpira mengi ni maamuzi ya kusikitisha sana.
Kwanza niwapongeze wale wote ambao wamefanikishwa kutiwa hatiani kwa klabu za Geita Gold Sports, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembwa, kwa hakika timu hizi nne zilistahili adhabu kubwa, lakini ninasikitika kuona wahusika wakuu wa ‘upangaji matokeo’ katika mechi za JKT Kanembwa 0-8 Geita Gold, Polisi Tabora 7-0 JKT Oljoro wakiachwa huru huku wengine kwa sababu tu TFF haikuwakilisha ushahidi wao katika Kamati ya Nidhamu ambayo ilitoa hukumu hiyo jana Jumapili.
Utawafungiaje magolikipa, Dennis Richard (Geita) na Mohamed Mohamed (JKT Kanembwa) na kuwatoza faini ya milioni kumi kila mmoja eti wamehusika katika upangaji wa matokeo na kuwaacha huru mwenyekiti wa chama cha soka cha mkoa Geita (Salum Kurunge,) mwenyekiti wa timu ya Geita Gold (Costantine Moladi,) na katibu mkuu wa JKT Kanembwa, (Basil Matei?). Huu ni ujinga mkubwa ambao kamati ya nidhamu ya TFF imeufanya.
Kama ningekuwa mimi na mamlaka ya urais wa TFF mara baada ya kutoa tamko kwamba TFF isingemtangaza mshindi wa kundi wa tatu katika ligi daraja la kwanza kwa sababu ya uwepo wa viashiria vya upangwaji wa matokeo katika michezo ya mwisho ya kundi hilo.
Ningekabidhi jambo hilo kwa mamlaka za kiserikali ambazo zinauwezo wa kuchunguza na kwa vile mambo ya rushwa yalihushwa moja kwa moja ni wazi ningewahitaji TAKUKURU waje washughulike na jambo hilo kwa kuwa ndiyo wenye mamlaka na uwezo huo.
Lakini kwa kuwa Jamal Malinzi (rais wa TFF) alihusishwa pia katika mchezo upangwaji wa matokeo ya gemu ya Kanembwa na Geita akaona ni tatizo hivyo akafanya ‘ujanjaujanja’ wa kupeleka jambo hilo kwa Kamati ya Nidhamu, ambayo si tu kwamba haina mamlaka ya kuchunguza mambo ya rushwa na kuwatiana hatiani watu, bali haina hata jino moja la kuweza kumkwangua yeye kama rais wa TFF.
Ili kujiweka salama zaidi, ‘marafiki zake’ wanaotuhumiwa pamoja akafanya waonekane wasio na hatia! Mchezaji na mchezaji, tena ni golikipa na golikipa tu wakishirikiana na kocha msaidizi wa Geita, Choki Abeid ambaye yeye masikini amefungiwa maisha yake yote kujihusisha na soka ndiyo walipanga matokeo katika gemu ya Kanembwa v Geita, ‘kituko cha kusikitisha.’
Hawa kamati ya Nidhamu wajinga kweli lakini ninachoshukuru ni kwamba tayari tumehakikishiwa kuwa matokeo yalipangwa kama ilivyoonekana. Haki ilikuwa ni kuzishusha timu hizo zote nne. Hakuna nchi ambayo inaweza kuruhusu mshindi wa gemu za Polisi Tabora v Oljoro na Kanembwa v Geita apande ligi ya kuu kutokana na aina ya mechi zenyewe zilivyochezwa.
Kuna msemo wa kale unasema, ‘ Mtu avukae nguo asipochutama chini hujitukanisha mwenyewe kwa kwenda uchi mbele ya watu.’
Maamuzi ya kuwakuta hatiani mwamuzi na mwamuzi wa akiba na kuwaacha huru katibu mkuu wa Polisi Tabora, Alex Kataya, katibu wa Oljoro, Hussein Nalinja na mtuza vifaa wa Polisi Tabora, Boniface Komba na meneja wa timu hiyo ni dalili nyingine ya ‘maamuzi ya kukatisha tamaa’ kwani waamuzi pekee hawawezi kufungisha 6-0, mechi ingevunjika.
‘Habari za kosa la mtu mkubwa ni wajibu kabisa kutangazwa katika ulimwengu kwa maandiko ya herufi kubwa na kwa wino safi.’ Mtu mdogo hana nafasi katika dunia hii ya kutenda jambo kubwa. Kidole changu bado nakinyoosha kwako rais wa TFF, Ndugu, Jamal Malinzi nahisi unacheza mschezo usio uweza.
CIA ndiyo wanawapeleleza na kuwatia hatiani wala rushwa wa FIFA! Hivi yule mtaalamu wa kupanga matokeo pale Italia yuko wapi? Polisi Tabora, JKT Oljoro, Kanembwa JKT na Geita Gold Sports zilistahili kushushwa hakika, lakini kamati ya nidhamu ya TFF ni wajinga kweli, wakawadanganye watoto wadogo, walioachwa huru ndiyo wahusika wakuu.
Hili jambo kamati za TFF hawaliwezi wasiipotezee muda wa maandalizi ya kucheza VPL msimu ujao timu ya Mbao FC. Halafu si kila kitu Waziri, Waziri kwani Waziri ndiye TAKUKURU? Hii issue imeanzia katika rushwa, na wale waliotoa na kupokea bado wapo huru, waliohukumiwa adhabu zao ziko sawa kabisa, kipa huwezi kususa, mwamuzi gani mechi ina simama zaidi ya dakika 15 kisha anaendelea kuchezesha?
Ila hawa watoaji rushwa mbona mmewaacha? Au kwa vile wapokeaji ndiyo nyie? ‘TFF imejichanganya sana katika sakata hili la rushwa/upangaji matokeo’

SOURCES ; SHAFFIH DAUDA

No comments:

Post a Comment